Kamanda wa Polisi mkoani humu, Ulrich Matei, amesema jana mjini Morogoro kuwa mtuhumiwa huyo aliandika taarifa hizo Agosti 27, mwaka huu kwa kutumia simu yake na kusambaza taarifa hizo kwenye kundi la mtandao wa Facebook.
Kwa mujibu wa Kamanda Matei, mtuhumiwa huyo aliandika ujumbe uliosomeka kuwa ‘Wanafanya mazoezi kwa ajili ya Ukuta, Polisi baadhi yao ni wema na wengine mjinga mijinga ife tu,’ maneno ambayo ni ya uchochezi dhidi ya jeshi hilo na wananchi.
Alisema mtuhumiwa huyo tayari ameshafikishwa mahakamani na kusomewa mashitaka.
Kamanda Matei amewaonya wananchi kuacha kuandika taarifa za uchochezi katika mitandao ya kijamii kwani wanakamatwa na kufikishwa katika vyombo vya sheria.
Pia amewatahadharisha wananchi kuwa makini na baadhi ya watu wanaofanya utapeli kwa kutumia majina ya viongozi wakuu waliopo mkoani humu, ili kujipatia fedha. Alisema wapo baadhi ya raia wasio wema, wanaotumia simu zao za mkononi kujitambulisha kwa baadhi ya wananchi kuwa wao ni viongozi na kutaka kutumiwa fedha kwa njia mtandao ya simu.
Alisema wameanza kufanya uchunguzi wa kuwabaini watu hao kwa kuzifuatilia namba zao za simu.
Aidha, aliwataka wananchi kutoa taarifa hizo pale wanapopigiwa simu na watu hao.
Pamoja na hayo, alisema Polisi mkoani Morogoro kwa kushirikiana na wenzao wa mikoa mingine inaendelea na msako wa watu wanaojihusisha na wizi wa magari. Alisema tayari watu wawili walishakamatwa jijini Dar es Salaam kwa tuhuma za kuhusika katika matukio hayo.
Chanzo-Habarileo